2 Chronicles 26:16-21

16 aLakini baada ya Uzia kuwa na nguvu sana, majivuno yake yakamsababishia kuanguka. Alikosa uaminifu kwa Bwana Mwenyezi Mungu wake, naye akaingia hekaluni mwa Bwana ili afukize uvumba kwenye madhabahu ya kufukizia uvumba. 17 bAzaria kuhani akiwa pamoja na makuhani wengine themanini wa Bwana wenye ujasiri wakamfuata huko ndani. 18 cWakamkabili na kumwambia, “Siyo sawa kwako, Uzia, kumfukizia Bwana uvumba. Hiyo ni kazi ya makuhani, wazao wa Haruni, ambao wamewekwa wakfu ili kufukiza uvumba. Ondoka mahali patakatifu, kwa kuwa umekosa uaminifu nawe hutaheshimiwa na Bwana.”

19 dUzia, ambaye alikuwa na chetezo mkononi mwake tayari kufukiza uvumba, akakasirika. Alipokuwa anawaghadhibikia makuhani mbele ya madhabahu ya kufukizia uvumba katika Hekalu la Bwana, ukoma ukamtokea penye kipaji chake cha uso. 20 eAzaria kuhani mkuu pamoja na makuhani wengine wote walipomtazama wakaona kwamba alikuwa na ukoma penye kipaji chake cha uso wakaharakisha kumtoa nje. Naam, hata yeye mwenyewe alikuwa anatamani kuondoka kwa sababu Bwana alikuwa amempiga.

21 fMfalme Uzia alikuwa na ukoma mpaka siku ya kufa kwake. Akatengwa katika nyumba ya pekee akiwa mwenye ukoma, naye akawa ametengwa kutoka Hekalu la Bwana. Yothamu mwanawe akawa msimamizi wa jumba la mfalme, pia akawaongoza watu wa nchi.

Copyright information for SwhKC